Deuteronomy 4

Waamriwa Utii

1 aSikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Bwana, Mungu wa baba zako anawapa. 2 bUsiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu ambayo nawapa.

3 cMliona kwa macho yenu wenyewe kile Bwana alichokifanya kule Baal-Peori. Bwana Mwenyezi Mungu wenu aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori, 4lakini ninyi nyote mlioshikamana na Bwana kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai mpaka leo.

5 dTazama, nimewafundisha amri na sheria kama Bwana Mwenyezi Mungu wangu alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki. 6 eZishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonyesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.” 7 fNi taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Bwana Mwenyezi Mungu wetu alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba? 8 gNalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?

9 hMwe waangalifu, na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke moyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.

10 iKumbuka siku uliyosimama mbele za Bwana Mwenyezi Mungu wako kule Horebu, wakati aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili kwamba waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.” 11 jMlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto mpaka mbinguni juu, pamoja na mawingu meusi na giza nene. 12 kNdipo Bwana alipozungumza nanyi kutoka moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu. 13 lAliwatangazia Agano lake na Amri Kumi, ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe. 14Naye Bwana alinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.

Kuabudu Sanamu Kwakatazwa

15 mHamkuona umbo la aina yoyote siku ambayo Bwana alizungumza nanyi kule Horebu kutoka kwenye moto. Kwa hiyo mjihadhari kwa uangalifu sana, 16 nili msije mkajichafua na kujitengenezea sanamu au kinyago chenye umbo lolote kama la mwanaume au mwanamke, 17 oau kama mnyama aliye juu ya nchi au ndege yeyote arukaye angani, 18au kama kiumbe kitambaacho juu ya ardhi au samaki yeyote aliye ndani ya maji. 19 pNa utazamapo juu angani na ukaliona jua, mwezi na nyota na vyote vinavyoipamba mbingu, usije ukashawishiwa kuviinamia na kuviabudu vile ambavyo Bwana Mwenyezi Mungu wenu alivyogawia mataifa yote chini ya mbingu. 20 qLakini kwenu ninyi, Bwana amewatoa kutoka kwenye tanuru ya kuyeyushia chuma, katika Misri kuwa watu wa urithi wake kama mlivyo sasa.

21 r Bwana alinikasirikia kwa sababu yenu na akaapa kwamba sitavuka Yordani kuingia katika nchi nzuri Bwana Mwenyezi Mungu wenu anayowapa kuwa urithi wenu. 22 sNitakufa katika nchi hii; sitavuka Yordani, lakini ninyi ni karibu mvuke mkaimiliki ile nchi nzuri. 23 tJihadharini msilisahau Agano la Bwana Mwenyezi Mungu wenu lile alilofanya nanyi; msijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote ambacho Bwana Mwenyezi Mungu wenu amewakataza. 24 uKwa kuwa Bwana aliye Mungu wenu ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.

25 vBaada ya kuwa na watoto na wajukuu na kuishi katika nchi hiyo siku nyingi, tena kama mkijichafua na kutengeneza sanamu ya aina yoyote, mkifanya maovu machoni pa Bwana Mwenyezi Mungu wenu na kumfanya awe na hasira, 26 wninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yenu siku hii kwamba mtaangamia mara moja kutoka nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki. Hamtaishi kule kwa muda mrefu bali kwa hakika mtaangamizwa. 27 x Bwana atawatawanya miongoni mwa mataifa, na ni wachache wenu tu watakaosalia miongoni mwa mataifa hayo ambayo Bwana atawafukuzia. 28 yHuko mtaabudu miungu ya miti na mawe iliyotengenezwa na watu, ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kula au kunusa. 29 zLakini kama mtamtafuta Bwana Mwenyezi Mungu wenu, mtampata; kama mtamtafuta kwa moyo wenu wote na kwa roho yote. 30 aaWakati mnapokuwa katika dhiki, nayo mambo haya yote yamewatokea siku hizo, ndipo mtamrudia Bwana Mwenyezi Mungu wenu na kumtii. 31 abKwa maana Bwana aliye Mungu wenu ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau Agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.

Bwana Ndiye Mungu

32 acSasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu mpaka mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa? 33 adJe, kuna watu wengine wowote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi? 34 aeJe, kuna mungu yeyote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu ya kutisha, kama yale ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu?

35 afMlionyeshwa mambo haya ili mpate kujua kuwa Bwana ndiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye. 36 agKutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonyesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kwenye ule moto. 37 ahKwa sababu aliwapenda baba zenu na alichagua wazao wao baada yao, aliwatoa katika nchi ya Misri kwa Uwepo wake na kwa uwezo wake mkuu, 38 aialiwafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi na kuwaleta ninyi katika nchi yao na akawapa ninyi kuwa urithi wenu, kama ilivyo leo.

39 ajKubalini na mweke moyoni leo kuwa Bwana ndiye Mungu mbinguni juu na duniani chini. Hakuna mwingine. 40 akMshike amri na maagizo yake ninayowapa leo, ili mpate kufanikiwa ninyi na watoto wenu baada yenu, na mpate kuishi maisha marefu katika nchi awapayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu siku zote.

Miji Ya Makimbilio

41 alKisha Musa akatenga miji mitatu mashariki ya Yordani, 42 amambayo mtu yeyote aliyemuua mtu angeweza kukimbilia ikiwa amemuua jirani yake bila kukusudia na bila kuwa na chuki naye siku zilizopita. Angeweza kukimbilia katika mmojawapo ya miji hii na kuokoa maisha yake. 43 anMiji hiyo ilikuwa: Bezeri katika tambarare ya jangwa kwa ajili ya Wareubeni; Ramothi katika nchi ya Gileadi kwa ajili ya Wagadi; nao mji wa Golani katika nchi ya Bashani kwa ajili ya Wamanase.

Utangulizi Wa Sheria

44Hii ndiyo sheria Musa aliyoweka mbele ya Waisraeli. 45Haya ndiyo masharti, amri na sheria Musa aliyowapa wana wa Israeli wakati walitoka Misri, 46 aonao walikuwa katika bonde karibu na Beth-Peori mashariki ya Yordani, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala Heshboni, naye alishindwa na Musa na Waisraeli walipokuja toka Misri. 47 apWaliimiliki nchi yake na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, wafalme wawili Waamori waliotawala mashariki ya Yordani. 48 aqNchi hii ilienea kutoka Aroeri ukingoni mwa Bonde la Arnoni mpaka Mlima Sioni (yaani Hermoni), 49pamoja na eneo lote la Araba mashariki ya Yordani, na kuenea mpaka Bahari ya Araba kwenye miteremko ya Pisga.
Copyright information for SwhKC